Home Kitaifa MHE. RAIS WA ZANZIBAR APONGEZWA KWA KUPANDISHA VIWANGO VYA PENSHENI

MHE. RAIS WA ZANZIBAR APONGEZWA KWA KUPANDISHA VIWANGO VYA PENSHENI

 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,kinampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,kwa maamuzi yake ya kupandisha viwango vya pensheni za wastaafu pamoja pensheni jamii kwa wazee wenye umri wa miaka 70.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis mara tu baada ya Rais Dk.Mwinyi, kutangaza viwango hivyo huko katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa yaliyofanyika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mbeto, amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa na imeandika historia kubwa katika falsafa ya utawala bora kwani mara nyingi wananchi wanaostaafu wamekwa hawapewi kipaumbele.

Alisema matunda hayo yanatoka na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ambayo imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kukuza uchumi ulitoa fursa ya kupatikana kwa fedha za kuimarisha miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuongeza pencheni hizo.

Alisema kuwa Dk.Mwinyi,ameendelea kuwa kiongozi mwenye maono,utu,huruma na mzalendo wa kweli katika kusimamia haki na kuimarisha maisha ya wananchi wa makundi mbalimbali nchini.

Tunampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa maamuzi yake ya kuongeza kiwango cha pencheni kwa wastaafu waliotumikia nchi kwa uadilifu mkubwa.

Hatua hii ni miongoni mwa mikakati,sera na vipaumbele vya CCM katika kuinua hali ya maisha ya wananchi wa makundi mbalimbali nchini”
,alisema Katibu huyo wa Kamati Maalum Mbeto.

Alifafanua kuwa maamuzi hayo ya kuongeza pencheni kwa wastaafu wa kima cha chini kwa asilimia 100 ambapo mstaafu aliyekuwa akipokea kiasi cha shilingi 90,000/= atapokea shilingi 180,000/= na kwa upande wa pencheni jamii imepanda kwa asilimia 150 kutoka shilingi 20,000/= hadi shilingi 50,000/= kwa Wazee wenye umri wa miaka 70.

Alieleza kuwa Dk.Mwinyi, mbali na kuongeza kiwango hicho cha pensheni pia ameahidi kuyafanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na Chama cha wafanyakazi Zanzibar.

Aidha,kupitia maadhimisho hayo Dk.Mwinyi alifafanua kwamba mabadiliko hayo ya pensheni yataanza katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar Khadija Salum Ali, alisema hatua hiyo ya Dk.Mwinyi ya kuongeza pensheni inatakiwa kuenziwa kwa vitendo kwani imejenga faraja na hamasa kubwa kwa wastaafu mbalimbali nchini.

Alisema kuwa kitendo cha kuongeza pensheni kwa wazee wenye miaka 70 ni hatua kubwa ya kimaendeleo kwani fedha hizo zitawasaidia kukidhi mahitaji yao mbalimbali ya kimaisha.

Tuendelee kumuunga mkono Dk.Mwinyi, kwani amekuwa ni kiongozi wa kutenda kwa vitendo sio maneno mengi tu bali anatekeleza ahadi zake kwa wakati”,alisema Khadija.

Kwa upande mkaazi wa kijiji cha Nungwi Said Issa Ame, alieleza kuwa kasi ya utendaji wa Dk.Mwinyi ni kubwa na amekuwa Rais wa nchi mwenye nia ya kuleta maendeleo katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!