Home Kitaifa Wataka Maadili Mema yafuatwe kwenye Jamii

Wataka Maadili Mema yafuatwe kwenye Jamii

CHUO cha Ukunga na Uuguzi Bukumbi kilichopo wilayani Misungwi kimewataka wanachuo wake kuenenda kwa maadili mema ya kitanzania ili waweze kufikia matarajio yao ya kutoa huduma kazini kwa wagonjwa kwa unyenyekevu pindi wamalizapo masomo.

Wito huo umetolewa jana katika Mdahalo wao uliokuwa ukizungumzia Mmomonyoko wa maadili katika sherehe za miaka 59 ya muungano wa Tanaganyika na Zanzibar kwenye chuo hicho kilichopo mkoani Mwanza.

Walisema vijana hawana budi kujitambua ili waweze kukabiliana na kuwepo kwa mmomonyoko unaoendelea kuikumba dunia kwa sasa ikiwemo Tanzania na hivyo kufanya baadhi ya vijana kukiuka utamaduni wetu.

Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bukumbi Lydia Chuwa alisema kuwa katika kipindi ambacho taifa linasherehekea miaka 59 ya Muungano wetu kuna vitu ambavyo vimeanza kupungua kwenye jamii hivyo kuna haja ya kujadiliana kuona namna ya kuepuka changamoto hizo.

Alisema kwa sasa kuna baadhi ya kaya mlezi ni mmoja kwa watoto baada ya kuwa wametengana, kuna suala la kuibuka kwa ushoga vitu hivyo vyote vinachangia kuporomosha maadili hapa nchini.

“Kuna haja kwa serikali kuanzisha mitaala ya maadili kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwani uadilifu utawafanya hata nyinyi mkahudumie vizuri wagonjwa” alisema Chuwa.

Mwanachuo mwaka wa tatu Jackline kimaro alisema kuporomoka kwa maadili ni matokeo ya umasikini ambapo baadhi ya wasichana hujikuta wakiuza miili yao ili kupata fedha huku wavulana wakijingiza kwenye ujambazi hivyo aliomba serikali kuanzisha mitaala ya kufundisha maadili.

Naye Daniel Richard alitaka serikali kuanzisha mitaala ya maadili kwenye shule zote kuanzia ngazi ya chini hadi juu ili kuwezesha vijana kuwa waadilifu, wenye kupenda utu na wenye kupenda kutunza utamaduni wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!