Na Shomari Binda-Musoma
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika(WiLDAF)limeitaka jamii kuachana na ukatili na kuwapa nafasi wanawake kumiliki ardhi.
Ujumbe wa shirika hilo umefikishwa na mwakilishi wa Konga ya kupinga ukatili wa kijinsi mkoani Mara inayosimamiwa na Wildaf,Robinson Wangaso,kutoka shirika la Vifafio kwenye kituo kimoja cha redio mjini hapa.
Akizungumzia mada isemayo,”ukatili wa kijinsia na umiliki wa ardhi kwa wanawake”amesema ukatili utakwisha iwapo kila mmoja atapaza sauti kupinga vitendo hivyo.
Amesema ukatili upo wa aina nyingi na umekuwa ukipeleka wahanga kuathirika kisaikolojia na wengine kupelekea ulemavu na vifo.
Wangaso amesema WiLDAF pamoja na wadau wake wamekuwa wakitoa elimu lakini ni jukumu pia la kila mmoja kufanya hivyo.
Amesema shirika hilo limekuwa likijihusisha na kuendesha mafunzo na mijadala mbalimbali kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na kuhamasisha wanawake kushiriki nafasi za uongozi.
Mwakilishi huyo amesema shirika linafanya kazi mikoa mingi hapa nchini kupitia miradi yake na limefika mkoani Mara kutoa ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili na kuhamasisha wanawake kumiliki ardhi.
“WiLDAF imekuwa ikifanya kazi kubwa pamoja na wadau wake kupinga masuala ya ukatili lakini hili ni jukumu la watu,taasisi binafsi na serikali katika kutokomeza vitendo hivyo.
“Jamii inapaswa kubadilika na kuchana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa nafasi kwa wanawake kumiliki ardhi”,amesema Wangaso.