Home Afya WAKRISTO 6147 WAFIKIWA NA ELIMU YA UGONJWA WA MARBURG KATIKA IBAADA YA...

WAKRISTO 6147 WAFIKIWA NA ELIMU YA UGONJWA WA MARBURG KATIKA IBAADA YA JUMAPILI.

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Ikiwa Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ikiendelea na juhudi mbalimbali za uelimishaji katika mkoa wa Kagera juu ya Ugonjwa wa Marburg, jumla ya waumini  elfu sita mia moja arobaini na  saba( 6147 ) kutoka makanisa mbalimbali ya Kikristo Bukoba mjini  na Wilaya ya Biharamulo  wamefikiwa na elimu hiyo wakiwa  katika sehemu za ibaada ya  kawaida  ya  siku za Jumapili.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Kengele tatu Bukoba Mjini ni miongoni mwa makanisa yaliyofikiwa na Waumini wake kupatiwa elimu ya Ugonjwa wa  Marburg  kukiwa na takriban jumla ya waumini 3019 walionufaika na elimu ambapo mwakilishi kutoka Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga, Elimu ya Afya kwa Umma  Beauty Mwambebule amehimiza washiriki kuendelea kuepuka tabia zinazoweza kuchochea maambukizi ya Marburg.

Tuepuke vitendo vinavyoweza kuchangia Maambukizi, kutosalimiana kwa kushikana mikono,tunawe mikono Kwa maji safi na tiririka na sabuni hasa ya maji, tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima, tukae Kwa kuachana nafasi, tunapoona dalili za ugonjwa huu kama vile kutokwa na damu Sehemu za wazi ,homa isiyo ya kawaida piga bure kwa namba  199 lakini tumshukuru Mungu hali sasa inaendelea vizuri hakuna Maambukizi mapya amesema Beauty  Mwambebule.

Halikadhalika, Kanisa la KKKT Usharika wa Kashura Bukoba jumla ya waumini  625 Wamefikiwa na Elimu  ya ugonjwa wa Marburg  ambapo  Mchungaji  wa Usharika wa Kashura  Mch.Alex Kasisi  ameishukuru Wizara ya Afya kwa kusema”Nashukuru sana Wizara ya Afya kwa kujali Afya za watu na kuamua kutembelea Kanisa letu kutoa ujumbe huu Mahsusi kuhusu ugonjwa huu wa Marburg, sisi kama kanisa hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha ujumbe huu unafika Kwa kila mshiriki”amesema .

Katika Kanisa la TAG Hamugembe  Bukoba Mjini jumla ya waumini 852 wamefikiwa na elimu ya tahadhari juu ya Ugonjwa wa Marburg, jinsi unavyoenezwa na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambapo  Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo Mch.Erasto Kyando amesema wao kama viongozi wa dini wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali  katika mapambano ya ugonjwa huo .

Tuendelee kumwomba Mungu aingilie kati juu ya Ugonjwa huu , sisi kama kanisa tupo tayari kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika mapambano ya ugonjwa wa Marburg na nashukuru sana jitihada zinazoendelea kufanywa na Wizara ya Afya ” amesema Mch.Erasto Kyando .

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Penford Joel amehimiza umuhimu wa kuripoti katika mamlaka husika pindi panapohisiwa kuna mtu ana maambukizi.

 “Kama kama kuna mtu yeyote anahisiwa anadalili za ugonjwa ni vyema kuripoti katika Mamlaka ya Serikali za mitaa Ili huduma ya Msaada wa haraka ufanyike “amesema .

Aidha, Penford ameongeza kuwa “Tuepuke Tabia ya kugusa maeneo tofauti tofauti kama hakuna ulazima kwani unaweza ukagusa Sehemu ambapo mwenzako amegusa na pana Maambukizi ya ugonjwa huo” amesema .

Pia, jumla ya waumini 327  Kanisa la EAGT Kahororo, Mlima wa Ahadi Bukoba Mjini wamefikiwa na kupewa elimu juu ya Ugonjwa wa Marburg.

Nao baadhi ya waumini wa makanisa mbalimbali ya Kikristo akiwemo  Mwalimu Shukuru Kyaka kutoka  Kanisa la KKKT Kengele tatu Bukoba mjini pamoja na Anchila Mkela wamesema hatua za Wizara ya Afya kuongeza nguvu ya uelimishaji itasaidia wananchi kuwa na uelewa Zaidi huku wakitoa ushauri kuongeza wigo hasa katika kuwaelimisha wananchi kuepuka misururu na misongamano mikubwa hasa kwenye misiba.

Mbali na makanisa  mbalimbali ya Bukoba Mjini kufikiwa elimu  baadhi ya makanisa yaliyopo  Wilaya ya Biharamulo yamefikiwa na kutolewa ujumbe mahsusi kuhusu Marburg ikiwa ni pamoja na   Kanisa la Roma  Catholic (RC) Kigango kata ya Kitendaguro  huku Waumini   895 wakipata elimu hiyo, Kanisa la AICT  Biharamulo  na jumla ya waliofikiwa ni  128,watoto 63 na watu wazima 65 ,Kanisa Katoriki  Biharamulo idadi ya waumini 310 wamepokea elimu juu ya ugonjwa wa marburg.

Makanisa mengine ni pamoja na  Kanisa la T.A.G Biharamulo ambapo jumla  ya waumini  207  wamefikiwa   huku KKKT Biharamulo ambapo jumla ya waumini  94 wamepata elimu juu ya ugonjwa wa mlipuko wa Marburg  huku kanisa la  FPCT Biharamulo maendeleo parish nao wakinufaika na elimu hiyo.

 Ikumbukwe kuwa timu ya wataalam wa Afya kutoka Wizara ya Afya wameweka Kambi mkoani Kagera kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzunguka maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko wa watu kwa kushirikiana na watalaam wa afya ngazi ya jamii hadi mkoa na kutoa elimu kwa njia ya vipindi kupitia Redio  Jamii zilizopo mkoani Kagera.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!