Home Kitaifa MHE. MAJALIWA AWATAKA MAAFISA HABARI KUTANGAZA UTALII WA TANZANIA KIMKAKATI

MHE. MAJALIWA AWATAKA MAAFISA HABARI KUTANGAZA UTALII WA TANZANIA KIMKAKATI

Na John Mapepele

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka Maafisa Habari wote nchini kuitangaza Tanzania ndani na nje mipaka yake kupitia vivutio mbalimbali vya utalii.

Mhe. Majaliwa ameyasema haya leo Machi 27, 2023 katika hotuba yake kwenye kikao cha 18 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali ambapo Rais wa Jamhuri wa Muungano Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo ya heshima kwa kutambua mchango mkubwa kwenye Sekta ya Habari.

Kikaoni hiki kimefanyika jijini Dar es Salaam katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere( JNICC).

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, Waziri Mkuu amesisitiza kuitangaza amani na fursa za uwekezaji zinazopatikana ikiwa ni pamoja na utalii na malikale.

Amewataka Maafisa Habari kuongeza ubunifu katika katika utendaji kazi huku wakiwa wazalendo kwa nchi yao katika kusukuma ajenda mbalimbali za maendeleo.

Aidha, amehimiza kutumia teknolojia katika kuvitangaza vivutio vya utalii huku akisisitiza kuendelea kutumia vikao kazi katika kubadilishana uzoefu.

Kwa upande mwingine amewataka kuhakikisha kuwa mambo yote yanayopangwa na Serikali yanafahamika na wananchi.

Lazima mhakikishe kila mwananchi anapata taarifa ya mipango ya Serikali, aidha ni muhimu kutoa taarifa sahihi kwa wakati.” Amesisitiza Mhe waziri Mkuu

Akitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa taasisi zote za Serikali amewataka kuhakikisha ikama za Maafisa Habari zinatimia ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha na kuwajengea uwezo.

Katika kikao hiki viongozi na wadau mbalimbali wa Serikali wameshiriki ikiwa ni pamoja Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Dkt Tulia Ackson, Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Mhe. Tabia Mwita na Katibu Mwenezi wa CCM Sophia Mjema na baadhi ya Makatibu Wakuu na viongozi waandamizi wa Serikali.

Takribani Maafisa Habari 600 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wameshiriki kikao hiki ambacho kifanyika kwa siku tano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!