Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema kuwa Bandari Kavu ya Kwala inatarajiwa kuanza kufanya kazi muda wowote kuanzia sasa na itatoa huduma zote za kiforodha kama zinavyotolewa katika Bandari zingine.
Akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, Meneja Miliki wa Mamlaka hiyo, Alexander Ndibalema ameeleza kuwa, kukamilika kwa bandari hiyo ni matokeo chanya ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imewezesha takriban Shilingi bilioni 83.247 kutumika katika kuendeleza bandari, ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka barabara kuu ya Morogoro eneo la Vigwaza kuelekea bandarini na kusogeza miundombinu ya reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3.
“Bandari Kavu ya Kwala ipo tayari kufanya kazi kwa sababu miundombinu yote ya msingi imekamilika na leseni zingine kutoka mamlaka zingine za Serikali zimeshakamilika ambapo kinachosubiriwa kwa sasa ni kupata leseni kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)”, alisema Ndibalema.
Ndibalema ameongeza kuwa, lengo kuu la kuanzisha bandari hiyo ni kuongeza ufanisi na kiasi cha shehena inayohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam, kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam, kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zitolewazo katika Bandari. Hivyo wateja kutoka sehemu mbalimbali wataweza kuchukulia mizigo yao ndani ya bandari hiyo ambayo ina uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na makasha 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.
Vile vile amefafanua kuwa, bandari hiyo ni ya kimkakati kwa sababu eneo la Kwala lina miradi mingi ya kimkakati ambayo imeanza kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa viwanda mbalimbali na ujenzi wa Mji mpya wa Kwala, hivyo ni matarajio kuwa mizigo ya Wawekezaji kutoka nchi mbalimbali inayokwenda kwenye viwanda itachukuliwa hapo.
Ameeleza kuwa, bandari hiyo inatarajiwa kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa ambapo sehemu kubwa ya mizigo itakayohudumiwa katika bandari hiyo ni ile inayokwenda nchi jirani.
Bandari hiyo imejengwa kwa awamu mbili zilizojumuisha usafishaji wa eneo lenye ukubwa wa Hekta 60 na ujenzi wa ukuta uliogharimu Shilingi 9,465,643,798.00, ujenzi wa Yadi hekta 5 kiwango cha zege uliogharimu Shilingi 36,670,971,842.00, ujenzi wa Reli Mchepuko yenye urefu wa KM 1.3 uliogharimu Shilingi 677,328,320.00 na ujenzi wa barabara yenye urefu wa KM 15.5 kwa kiwango cha zege uliogharimu Shilingi 36,432,867,115.70 ambayo imekamilika kwa asilimia 100.