Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuanzia Januari mwaka 2020 hadi Desema, 2022 jumla ya ajali 5132 zilizoripotiwa kwenye vyombo vya usalama na kutolewa taarifa na jeshi la polisi ziligharimu maisha ya watu 4060 na kusababisha majeruhi na walemavu 6427.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa takwimu hizo leo jijini Mwanza wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika Kitaifa Katika Uwanja wa Furahisha Uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Amefafanua kwamba abiria 1582 walipoteza maisha, 4372 walipata majeraha ikiwemo ulemavu, watembea kwa miguu 959 walipitiwa na vyombo vya usafiri walipokuwa wakitembea, 650 walijeruhiwa, wapanda pikipiki 797walipoteza maisha, 725 walijeruhiwa, wapanda baiskeli 196 walipoteza maisha 82 walijeruhiwa, madereva 509 wanaoendesha vyombo vya moto wamepoteza maisha 584 wamejeruhiwa na watembeza mikokoteni 17 wamepoteza maisha 14 walipata madhara.
Kutokana na takimu hizo ambazo zinagharimu maisha ya watanzania na kupoteza nguvu kazi ya taifa, Majaliwa ametoa maagizo 13 kwa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ikiwemo kuharakisha mchakato wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwa na sheria bora isiyoacha mwanya kwa watumiaji wote wa barabara wanaotembeza vyombo bila kuzingatia sheria.
Aidha amelitaka Baraza hilo kufuatilia kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka alama kwenye barabara na leseni za udereva ili kuwabaini madereva wanaokiuka sheria na iwe rahisi kuwachukulia hatua, jeshi la polisi Tanzania liharakishe ufungaji wa mifumo ya kielektroniki itakayokuwa inabaini makosa mbalimbali ambayo inasaidia kulinda mwenendo wa madereva wasiokuwa na maadili na pia itarahisisha ufanyaji kazi maana itatoa taarifa ni dereva yupi anayeendesha vyombo vya moto akiwa amelewa.
“Pia Baraza litekeleze kwa ukamilifu maagizo ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye maadhimisho ya wili ya nenda kwa usalama barabarani mwaka jana 2022 yaliyofanyika jijini Arusha kuhusu kuimarisha ukaguzi wa magari kwa kushirikisha sekta binafsi badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha jeshi la polisi peke yake kukagua magari maana magari ni mengi,”amesema Mhe. Majaliwa na kuongeza
Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa Uaslama Barabarani mwaka huu yanaongozwa na Kauli Mbiu isemayo ’Tanzania bila ajali inawezekana -Timiza wajibu wako’
Mwisho