Home Michezo MAKOCHA 25 WANOLEWA DIPLOMA B CAF

MAKOCHA 25 WANOLEWA DIPLOMA B CAF

Na Boniface Gideon, TANGA

JUMLA ya makocha 25 wapo mkoani Tanga wakipatiwa mafunzo ya ukocha ngazi ya Diploma B ya CAF inayoendeshwa na shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’ hii ikiwa ni jitihada moja wapo zinazofanyika kukuza na kuboresha soka hapa nchini pamoja na kuwajengea uwezo utakaowasaidia kuingia katika soka la ushindani.

Kozi hiyo ya siku 10 ambayo imeanza February 28 hadi Marh 9,2023 imejumuisha pia raia wawili wa kigeni kutoka Rwanda na Kenya ambapo mara baada ya washiriki kuhitimu watapata nafasi ya kwenda kushiriki kozi ya leseni A ya shirikiho la soka Barani Africa ‘CAF’ sambamba na kupewa fursa ya kwenda kuwa wasaidizi kwenye mabenchi ya timu mbalimbali hapa nchini.

Kozi hiyo ambayo inafanyika katika kituo cha michezo kinachojengwa na TFF kilichopo Mnyanjani jijini Tanga imehudhuriwa pia na baadhi ya wachezaji wa zamani waliowahi kuzichezea timu mbalimbali hapa nchini akiwemo Mussa Hassan Mgosi, Nizar Khalfan, Abdi Kassim , Aggrey Morris, pamoja na Kali Ongala.

Akifungua mafunzo hayo Rais wa shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Walles Karia alisema kuwa mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanawatumia wachezaji wa zamani waliowahi kucheza kwa nyakati tofauto tofauti hapa nchini kuwapa fursa ya kupata kozi hizo ili kuziongoza timu zinazoshiriki ligi mbalimbali za ndani ikiaminikma kuwa wao watakuwa ni chachu na mchango mkubwa wa kuzidi kukuza vipaji kwa wachezaji na kuzisaidia timu za taifa katika michuano ya kimataifa.

Ni faraja kubwa sana kwa sababu kozi hii imejumuisha wachezaji wengi wa zamani kwa maana wametambua kuwa wao baada ya uchezaji wao wameendelea kufundisha lakini pia wanataka wafundishe wakiwa wenye sifa na vigezo vinavyostahili ninawapongeza kwa hilo”

“Lakini pia ni utaratibu wetu sisi TFF kuhakikisha kwamba tunawatumia wachezaji wa zamani kwa sababu wametumikia mpira muda mrefu na wamepitia katika mifumo ambayo ipo nchini kwetu na wanatambua hali halisi na mazingira kuhakikisha kwamba mchezaji asije akasikitika kwamba muda wake umeisha bado anang’ang’ania kucheza mpaka ligi ya wilaya ajitambue kwamba anaweza akatumika katika sehemu nyingine yeyote ile ikiwemo kusaidia katika timu zetu za Taifa” alisema Rais Karia.

Alisema mpaka sasa bado ipo changamoto ya makocha wa Tanzania kushindwa kufundisha soka nje ya mipaka ya Tanzania hii ikichangiwa pia na kukosa vigezo stahiki hata hivyo ni matamanio makubwa ya TFF kuona wanaendelea kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuendesha kozi mbalimbali zitakazoweawezesha makocha kuingia katika soka la kiushiundani ndani na nje.

“Suala la makocha wetu kwenda kufundisha nje ya nchi bado ni changamoto ambayo ipo lakini huko nyuma walishawahi kwenda sasa hivi tunataka hii hali ambayo makocha wanakuja Tanzania na wa kwetu hawatoki ije ibadilike lakini haiwezi kubadilika kama wao wenyewe hawatakuwa na vigezo vinavyostahili” aliongeza Rais Karia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!