Asila Twaha, OR – TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. David Silinde amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi (miundombinu), Wakuu wa Idara za Miundombinu na Maendeleo Vijijini na Mijini wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameneja wa TARURA Mikoa na Wilaya kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi ili kuweka kumbukumbu sawa.
Mhe. Silinde amesema hayo Februari 20, 2023 Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa kazi wa Makatibu Tawala Wasaidizi Sekretarieti za Mikoa(miundombinu), Wakuu wa Idara za Miundombinu na Maendeleo ya Vijijini na Mijini katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mameneja wa TARURA Mkoa na Wilaya.
Ameeleza wapo baadhi ya watendaji sio wakweli pindi wanapoulizwa hatua ya utekelezaji wa miradi ilipofikia hawasemi ukweli na hii huonesha kutowajibika katika kazi zao na kutoleta picha nzuri pindi viongozi wanapofika kukagua miradi hiyo na kukuta utekelezaji wake hauendaji na maelezo yaliyotolewa awali hiyo ni ukiukwaji wa misingi ya utumishi wa umma.
Amefafanua kama kiongozi ukiaminiwa ni vizuri kuwa na uwaminifu kwa watu unaowatumikia ambao ni wananchi.
Mhe. Silinde amewataka watendaji hao kutekelea majukumu yao na kuwa na takwimu sahihi za kiutendaji pale zinapohitajika.
“huwezi kuchelewa bila sababu ukitoa taarifa sahihi hamna mtu atakuhukumu” amesema Mhe. Silinde
Aidha, amewataka watendaji hao kutekeleza ahadi za viongozi kwa kutenga bajeti katika mipango yao ili kuendana na kasi ya Serikali lakini pia kuwataka kutangaza kazi zilizofanyika ili kutoa uelewa kwa wananchi.
Kikao hicho kiliwashirikisha wajumbe zaidi ya 300 na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki.