Na Boniface Gideon, TANGA
Wananchi wa Mtaa wa Kongwa Kata ya Mzizima katika Halmashauri ya Jiji la Tanga mwishoni mwa Wiki wamemlalamikia mwekezaji wa Xuanyi Company Limited ya China kuvamia chanzo cha maji cha mto Amboni kwa kuanza kuchimba Udongo na kuharibu Mazingira bila kupata Vibali kutoka Serikalini.
Maeneo hayo yaliyovamiwa na mwekezaji huyo yalikua yakitumika na wananchi kwa ajili ya kilimo cha Bustani na matunda ambayo yalikua yanawaingizia kipato na kufanya ulinzi katika vyanzo vya maji.
Inadaiwa kuwa kampuni hiyo ilivamia eneo Hilo lenye maji mengi ya chemchem mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka Jana na kuanza kuchimba mchanga kwaajili ya Ujenzi wa Bandari ya Tanga bila kupata Vibali kutoka Serikalini,
“Sisi tuliona makatapila yanaletwa na wakaanza kutengeneza Barabara yakupita magari ya mizigo, Baada ya hapo wakaanza kuchimba mashimo kwenye magugu maji tuliyoyapanda kwaajili ya kutunza chanzo Cha Maji, wakavunja na kuharibu miti yetu ya matunda pamoja na Bustani za mboga , tulipouliza walijibu kuwa ni Serikali imeamua kuchimba mchanga kwaajili ya Ujenzi wa Bandari, sisi Kama Wananchi hatukuwa na jinsi tuliridhika Mana kama Serikali imeamua kuchimba mchanga sisi hatuwezi kuizuia ” Alisema Meshack Mtasiwa mmiliki wa eneo la chanzo Cha Maji.
kwaupande wake Abdala Athuman aliselema kuwa kwa sasa hawana shughuli za kufanya katika eneo hilo na limekua hatari,kwani mvua iliyonyesha hivi karibuni,maji yanayotoka milimani yalipasua ukingo wa mto na kuhamia eneo lililokuwa linachimbwa udongo,
“Kiukweli hapa kwa sasa Mazingira yameharibiwa Sana Maana amevunja na kuharibu eneo la chanzo kikuu Cha Maji ambacho sisi tulipanda miti na magugu maji na kiukweli hapawezi kurudi kwenye Hali yake lakini pia sisi wenyewe Maisha yetu yamekuwa magumu kwakuwa Bustani zetu za mboga na matunda zimeharibiwa na ameacha shimo kubwa ambalo haliwezi kurudi kwenye Hali yake ya kawaida hata akisawazisha” Alisisitiza Athumani
Malamiko hayo yalifika kwa wasimamizi wa vyanzo vya Maji na kutoa vibali(Bonde la Mto Pangani) na kufanya ziara ya gafla na kukuta hali ikiwa ni mbaya kwa uharibifu wa ardhi ulivyofanyika na kuchukua hatua za haraka kwa kuzuia magari yote yaliyokuwepo kwenye eneo hilo la uchimbaji,malori mawili ya kubeba udongo na Catapiller moja ya kuchimba zilizuiliwa,na eneo lote kuzungushiwa uzio ili wasiendelee na uchimbaji
Akizungumza na Waandishi wa Habari mtaalamu wa Maji chini ya ardhi kutoka Bonde la Mto Pangani,Mitinje Lubegu alisema waharibifu wa vyanzo vya maji hawatakiwi kuvumiliwa kwa sababu wanasababisha madhara makubwa kwenye utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
“Hawa watu hawatakiwi kuvumiliwa kwa kuwa wanaharibu vyanzo vya maji,tumefika hapa tumezuia kwa mujibu wa sheria za raslimali za maji namba 11 ya mwaka 2009,ambayo imefanyiwa marekebisho ya sheria namba 8 ya mwaka 2022,ambazo zinakataza shughuli yeyote ya kibinadamu kufanyika ndani ya mita 60 kutoka chanzo Cha Maji” alisema Mitinje
Ikumbukwe kuwa januari 12 mwaka huu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alipotembelea bwawa la Mabayani na kujione uchafuzi wa Maji,aliwaagiza Bonde la Pangani kuwatafuta wanaovamia maeneo ya vyanzo vya Maji na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kukiuka taratibu za utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mwisho