Home Kitaifa JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA ILALA NA KUSINI UNGUJA WAPONGEZA MRADI WA...

JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA ILALA NA KUSINI UNGUJA WAPONGEZA MRADI WA RELI YA KISASA SGR

Katika kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ya Chama Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na wenzao wa Wilaya ya Kusini Unguja, Zanzibar leo tarehe 23 Disemba 2022 wametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya SGR kuanzia Dar es Salaam mpaka Pugu.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Ilala Ndugu. Mohamed Ramadhani Msofe amesema wameridhishwa na kazi inayoendelea na wanampongeza Rais na Mwenyekiti wa Chama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyosimamia ilani ya Chama cha Mapinduzi

“Tumejionea wenyewe jinsi mambo yalivyo hapa Mhandisi ametupitisha kuanzia hapa jengo la Tanzanite, tumeona mfumo wa umeme unavyofuliwa na jinsi treni zitakavyoongozwa na tumefika mpaka kituo cha Pugu kuyaona Mabehewa yenyewe kwakweli kazi imefanyika” alisema Msophe.

Aidha Mwenyekiti huyo wa Wazazi Wilaya ya Ilala amesema hata kama kuna propaganda za watu wasioitakia mema nchi yetu lakini wao jukumu lao ni kutoa elimu na kwa jinsi walivyoona basi watatoa elimu kwa kila mtanzania mwenye kutaka kuelewa.

“Lakini pia nitoe shukrani kwa Mwenyekiti wetu Dkt. Samia na wasaidizi wake wote, pia kwa watendaji wote wa shirika la Reli kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia ujenzi huu wa reli ya kisasa SGR na naahidi sisi kama Wazazi Wilaya ya Ilala tunakwenda kutoa elimu kwa jamii kwamba jinsi gani Serikali inafanya kazi zinazoonekana na zilizonyooka” alisisitiza Ndugu Msophe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kusini Unguja Ndugu. Abdallah Haji Makame amesema wao wana urafiki na wenzao wa Ilala na hii sio mara ya kwanza kuja lakini safari hii wamepata mafunzo makubwa hasa kutembelea mradi huu wa reli ya kisasa SGR.

“Hapa tumeona utekelezaji wa ilani ya CCM na juhudi anazofanya Rais wetu wa awamu ya sita amejitahidi sana, hapo nyuma hatukuwa na maendeleo kama haya” amesema Makame.

Pia akizungumzia utendaji kazi wa Rais Samia Ndugu. Makame amesema kwa kipindi kifupi sana ameweza kutekeleza miradi mingi iliyokuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Akizungumzia mradi wa SGR Mwenyekiti huyo wa Wazazi Wilaya ya Kusini Unguja amesema wamejionea wenyewe maendeleo makubwa ya ujenzi wa Reli hiyo kuanzia Dar es Salaam mpaka Pugu na kutoa sifa kwa Mabehewa akisema ni ya kisasa na yanaonekana yako imara na yana uwezo wa kufanya kazi tofauti na Wapinzani wanavyosema.

“Reli hii itakapoanza kufanya kazi nina uhakika itakuza uchumi wa nchi na kusaidia sana katika sekta ya Usafirishaji wa mizigo na binadamu hiyo kuongeza pato kwa Taifa na mtu mmoja mmoja” amesema Ndugu. Makame.

Wakichangia kwa nyakati tofauti Bwana. Mzee Ally Pira. Mjumbe wa Baraza kuu Wazazi Taifa amesema wao wamekuja kujifunza na kwa jinsi walivyouona mradi wa reli ya SGR wamethibitisha kabisa ilani ya Chama cha Mapinduzi imetekelezwa.

“Kwakweli lazima tuseme Mhe. Rais kwa kipindi kidogo alichokuwa madarakani amefanya kazi kubwa sana huu ni mradi mkubwa na amefanya kwenye Shule, vituo vya afya, Barabara, Maji na vingine vingine vingi lazima tumpongeze Rais wetu” alisema Bwana. Pira

Naye Bi. Fatma Suleiman Mtego. Mjumbe wa Kamati ya utendaji Wazazi Wilaya ya Ilala amesema kwa jinsi mradi wa reli ya kisasa SGR hatua uliyofikia hakuna la zaidi ila ni kweli Mama Samia chini ya Uongozi wake hakuna kilichosimama na hata miradi yote iliyoachwa na Marehemu Rais Magufuli, Mhe. Rais Samia ameendeleza kwa kasi tena zaidi kilichopo ni kumuombea kwa Mungu ampe nguvu zaidi ili awatumikie Watanzania.

Kuhusu mradi wa SGR Bi. Fatma ameendelea kusema kuanzia Jengo la Tanzanite, reli yenyewe na hata mabehewa ya treni yeye binafsi amejionea mambo makubwa sana ambayo hakutegemea kama yanaweza kutokea Tanzania hivyo anampa hongera sana Rais na Mwenyekiti wa Chama kwa kazi kubwa aliyoifanya.

“Humu ndani kwenye hili jengo la kituo cha Dar es salaam kuna vitu nimeviona hata sielewi nielezeeje, yani kuna sehemu unaingiza pesa unaweka na kiwango halafu unarudishiwa na chenji yani hayo yote yanafanywa na mashine, kwakweli sijawahi kuona” alisema Bi. Fatma.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!