Home Kitaifa WATU 11 MBARONI KWA TUHUMA ZA UHALIFU MITANDAONI

WATU 11 MBARONI KWA TUHUMA ZA UHALIFU MITANDAONI

Na Magrethy Katengu

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na timu maalum ya kuzuia na kupambana na makosa ya mtandao limewakamata watuhumiwa 11 wa makosa ya kimtandao.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Jumanne Muliro amesema kukamatwa kwa wahalifu hao ni kufuatia ufuatiliaji mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na Timu hiyo Maalum

Kamanda Muliro amesema kufutia msako huo Jeshi la Polisi na timu hiyo, limemkamata Alex Magoti (26) Mkazi wa Tabora Mjini na wenzake nane kwa tuhuma za kumiliki luninga za mtandaoni na akaunti za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa za uongo au uzushi kuhusu Viongozi wakubwa wa Serikali ikiwemo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,Hayati Dkt John Pombe Magufuli na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete hivyo kuleta taharuki kwa jamii

Watuhuhumiwa hawa wamekuwa wakiweka taarifa zao za uzushi, uongo na upotoshaji kwenye luninga za mtandaoni zinazotambulika kwa majina ya BSUN Online TV, GATTU Online TV, TAMUTAMU online TV, KILIMANJARO online TV na nyinginezo. Mfano wa taarifa hizo ni kama “Rais Samia akosoa vikali utawala wa Rais JPM, aanika ukatili aliofanya (haukubaliki hata kidogo)”, amesema ACP Muliro

ACP Muliro amesema Jeshi la Polisi limemkamata, Joseph Mzava (19) mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo cha Biachara Dar es Salaam (CBE), kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao kwa kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.

Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema wanamshikilia Li Naiyong (48) raia wa China, ambaye anatuhumiwa kujihusisha na shughuli za kuingilia mfumo wa mawasiliano kinyume na taratibu za nchi, na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Shilingi Milioni Mia mbili ishirini na moja laki moja sitini na tatu na mia sita (Tshs 221,163,600)

Pia Mtuhumiwa huyo amekuwa akituma vifaa visivyo rasmi kuwaunganisha watu kwa simu kufanya mawasiliano nje ya nchi kinyume na sheria za Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA.

“Watuhumiwa wote wapo chini ya Jeshi la Polisi saa yeyote watafikishwa Mahakamani kujibu zinazowakabili hivyo kama kuna wengine wanaendelea kuiga na kufanya matukio kama haya waache mara Moja” amesema Kamanda

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa za uongo na zile zitakazo zua taharuki kwa umma, Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu/watu wote watakao vunja sheria, kanuni na miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya mitandao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!