Na Magrethy Katengu
Chama Cha Wafanyabiashara ndogondogo Maarufu kama Wamachinga Mkoa wa Dar es salaam wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada za kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi zao ikiwemo kuwaweka kwenye mpangilio mzuri pamoja na kujenga masoko ya kisasa.
Akizungumza na Waandishi wa habari Leo Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dar es salaam Namoto Yusufu Namoto amesema kuwa mwaka 2022 Wamachinga wamepata mafanikio mengi ikiwemo kutambuliwa na serikali na kutengewa maeneo maalumu kwa ajili ya kufanya biashara zao.
Hata hivyo amesema sasa serikali imekua ikiwashirikisha kila jambo linalowahusu Wamachinga hali ambayo inasaidia kuondoa malalamiko kusaidia kusikiliza mahitaji yao ya msingi ikiwemo kuboreshewa miundo mbinu ya masoko ya biashara kwa nakuondoa dhana machinga ni mtu alie kata tamaa.
“Serikali imekuwa ikitushirikisha kwa kila jambo linalotuhusu,nasisi tumekuwa tunafurahi tunapoona maombi yetu yanafanyiwa kazi, mfano kwa sasa halmashauri zote zinajengewa soko jipya la kisasa na masoko mengine yanakarabatiwa mfano Wilaya ya Ilala kuna soko la Kisutu, Kinondoni soko la Magomeni nakadhalika, hivyo ni jambo la kufurahisha sana kwetu” amesema Namoto.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Wamachinga Mkoa wa Dar es salaam ameendelea kusema kuwa kwasasa wamachinga wamekuwa wakiaminika zaidi kwenye taasisi za kifedha ikiwemo mabenki ambapo wanapata mikopo yenye riba nafuu ya kuendesha shughuli zao za kibiashara .
Akizungumzia Changamoto walizokumbana nazo mwaka huu 2022 Namoto amebainisha kuwa wamepatwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya masoko kuungua moto ambayo ni Soko la Kariakoo, Karume, Vetenari, Soko la Cocacola nakwamba hali hiyo imewafanya baadhi ya wafanyabiashara waweze kukata bima ya Majanga endapo ikitokea ajali ya moto waweze kupata fidia.
“Niseme tu Wamachinga ni kundi kubwa sana na wengi wao hawajasoma kipindi cha Rais Hayati Dkt John Pombe Magufuli alisema msiwabugudhi Wamachinga waacheni wafanye biashara popote huku mkiwatafutia utaratibu mzuri hivyo alipoingia Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akateleleza kuwawekea utaratibu namna ya kufanya biashara hivyo angalau wakaondoka Barabarani na kwenda maeneo mengine”amesema Namoto
Hata hivyo amebainisha Matarajio ya Mwaka 2023 Namoto amebainisha kuwa Chama Cha Wamachinga Mkoani humo kitahakikisha Wamachinga wote wanapatiwa Vitambulisho,lakini pia kuanzisha vikundi vya ujasiliamali kuhusu Kilimo Cha aina mbalimbali ikiwemo matunda na chakula Ili kuhakikisha wanazalisha mazao ambayo yatatumika kuuzwa kwenye masoko mbalimbali.
“Tuna program yakuanzisha vikundi vya ujasiliamali katika sekta ya Kilimo ,pia Wamachinga tutawapeleka kwenye vyuo vya ufundi wajifunze kutengeneza vitu mbalimbali mfano nguo za batiki,hii itasaidia kuondokana na fikra za Wamachinga kudhani kwamba umachinga ni kuuza bidhaa Barabarani tu,kumbe Wanaweza kufanya ujasiliamali Kwa njia nyingine” amesema Namoto..
“Tayari tumefanya tafiti mbalimbali Kwa Kilimo Cha matunda aina ya tikitimaji ,Nanasi huko bagamoyo, ,na Kilimo Cha mpunga Morogoro,hatua hii ni kuwezesha Wamachinga wanaopenda kufanya ujasiliamali wa Kilimo tuwapeleke huko waweze kuzalisha chakula na matunda“amesisitiza Namoto.
Aidha tunaendelea kumshukuru Mungu Kwa yote yaliyotokea mwaka 2022 na tunaiahidi Serikali tutashirikiana nayo bega kwa bega huku tukifanya shughuli zetu kulingana na utaratibu tuliopewa