Taasisi ya The Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na UN Women na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia , wanawake na makundi maalumu imekutana na wadau na makundi mbalimbali kwaajili ya kukusanya maoni ambayo yatatumika kukamilisha mpango wa kitaifa wa kumlinda Mwanamke.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo Disemba 21,2022 Jijini Dar es salaam Afisa utawala na fedha wa Taasisi hiyo Erica Kiduko amesema kuwa mpango kazi huo una faida kubwa haswa katika kuangalia namna ya kumlinda mwanamke , mtoto na msichana katika madhila tofautitofauti.
“Tunaangalia ni jinsi gani ya kumlinda Mwanamke, mtoto, msichana na endapo Mwanamke anapopata madhira tofauti tofauti kama kubakwa, unyanyasaji wa kijinsia je ni haki gani za kumpatia ahueni”.
Hata hivyo ameeleza kuwa wataendelea kukusanya maoni mbalimbali kutoka ka wadau hao Jijini Dar es salaam kwa siku mbili ikifatiwa visiwani Zanzibar na sehemu zingine kwani zoezi hilo litaendelea kukusanya maoni zaidi kwa kukutana na watu mbalimbali.
Aidha, Mkurugenzi wa Shirika la Global Peace Foundation Tanzania, Martha Nghambi amesema mkutano huo ni fursa kwa vijana kutoa maoni namna sahihi ya kuhakikisha vijana wanapata uelewa wa kuhakikisha mtoto wakike anapata uhuru na amani katika shughuli zake za kila siku.
“Jukwaa muhimu kwa vijana zaidi kwani utaweza kuweka muelekeo na mwangaza wa jinsi gani wanaweza wakatekeleza kikamilifu yale ambayo wameyapanga kuweza kuyatekeleza katika maeneo mbalimbali.”
Aidha Nghambi amesema tangu kuanza kwa mpango mkakati kama huo hadi sasa kumekuwa na matokeo chanya ndiyo maana wamewiwa kuendeleza na kuja na mpango mkakati huo wa Taifa kwaajili ya wanawake, amani na usalama.
“Matokeo chanya yamepatikana kwa ngazi ya awali had sasa tulipofikia, lakini pia tumefanikiwa kufanya uchunguzi kujua kuna mapungufu gani na matatizo yaliyopo kwenye ripoti ili tuweze kuyatatua na kuweza kufika pale tulipofika”