
📌 Lengo ni kuyafanya makampuni ya usambazaji mafuta upande wa Kaskazini kutumia Bandari ya Tanga.
📌 Asema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.
📌Kapinga asema Tanga ni Mkoa muhimu katika sekta ya nishati nchini.
📌Uwekezaji huo unaunga mkono na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Nishati kufanya mapitio ya sera ya usafirishaji wa mafuta nchini ili kuyawezesha makampuni yanayosambaza mafuta ukanda wa Kaskazini kutumia Bandari ya Tanga kupitia GBP.
Rais Samia ameyasema hayo leo machi 1, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa ghala la kupokelea gesi ya kupikia ya LPG katika kampuni ya BGP ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo mkakati unasema ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Hii kazi wanaifanya vizuri sana wao kama GBP, lakini wale ambao wanachukua mafuta kwa ajili ya usambaza ukanda huu, au kupeleka nje ya nchi kupitia kaskazini bado wanachukulia mafuta Dar es Salaam, nendeni mkafanye mapitio ya Sera”. Aliagiza Dkt. Samia.

Dkt. Samia amesema GBP Tanga inayo mafuta ya kutosha kusambaza kanda ya Kaskazini pamoja na Nchi zilizo ukanda wa kasikazini hivyo hakuna sababu ya wasambazaji hao wa mafuta kuyachukulia Dar es Salaam.
Aisha, Rais Samia ameipongeza GBP kwa hatua iliyochukua ya kuanzisha vituo vya kujaza gesi kila Mkoa na kuongeza kuwa Serikali inaunga mkono uwekezaji huo.
Amewahakikisha wawekezaji Serikali kuweka Sera rafiki na endelevu zitakazotabirika na sera zitakazowawezesha wawekezaji wa Tanzania kuwa washindani katika soko la ndani na soko la kimataifa.

Awali Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema Jiji la Tanga ni muhimu ndani ya sekta ya nishati kwani ndio kitovu cha kupokea na kusambazaji wa mafuta Mikoa ya Kaskazini na Nchi za Ukanda wa Kasikazini.
“Wenzetu wa GBP ni washirika wa kiuchumi wa sekta ya nishati hususani kwenye sekta ndogo ya mafuta kwa sababu maghala yao ndio yanatumika kupokea na kusambaza mafuta kwa upande wa Kaskazini”. Amesema Mhe. Kapinga.
Mhe. Kapinga amempongeza Rais kwa kuweka chachu na msukumo wa Sera nzuri katika uwekezaji ambazo zinawafanya wawekezaji hao waendelee kuwekeza katika sekta ya nishati.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TIC imekuwa iki support wawekezaji kwa kuchukua hatua za kikodi ambazo zimekuwa rafiki ikiwa ni pamoja na uondoaji wa kodi za ongezeko la thamani kwenye vifaa vya LPG

Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa sera nzuri za uwekezaji zilizopo zimewaongezea hari wawekezaji wa ndani wa kuwekeza kitokana na kuweza kudhindana na wawekezaji wanaoleta vifaa kutoka nje ya Nchi.
Aidha, kutokana na mfumo wa soko uliopo katika nishati safi ya kupikia viwanda vimekuwa vikiongezeka vya utengenezaji wa gesi za majumbani.
